MHE. BALOZI FREDRICK I. KIBUTA AKUTANA NA WAWAKILISHI WA TAASISI YA BUSINESS RUSSIA YA SHIRIKISHO LA URUSI
Mnamo tarehe 23 Machi 2022 Mhe. Balozi Fredrick I. Kibuta pamoja na Maafisa wa Ubalozi walikutana na Wawakilishi wa Taasisi isiyo ya Kiserikali ya hapa nchini Urusi. Taasisi hiyo inajulikana kama "Business Russia".  Kutoka upande wa Business Russia, wawakilishi walikuwa wajumbe wafuatao:
1. Bw. Yuri Korobov - Mjumbe wa Bodi wa Taasisi hiyo na Balozi wa Biashara nchini Tanzania;

2. Bw. Anthon Silichenko - Mkurugenzi wa Kitengo cha Ushirikiano wa Kimataifa; na

3. Bi. Dariga Muhamedina - Meneja Miradi Kitengo cha Ushirikiano wa Kimataifa.
Taasisi ya Business Russia ni kiungo muhimu kati ya Jamii ya wafanyabiashara/wawekezaji na Taasisi za Serikali ya Shirikisho la Urusi zenye dhamana ya kusimamia Biashara, kwa mfano Mabaraza ya Biashara na Wizara za Maendeleo ya Uchumi, Viwanda na Biashara. Aidha, mpaka sasa taasisi hii ina wanachama wafanyabiashara zaidi ya 1000, mabalozi wa biashara 36 katika nchi mbalimbali duniani, na katika Bara la Afrika wana mabalozi nchini Tanzania na Afrika ya Kusini. Vilevile ndani ya mfumo wao wana kamati 32 zinazoshughulikia masuala ya Uchumi wa Viwanda. Sambamba na hilo wana matawi katika majimbo yote 84 ya Shirikisho la Urusi pamoja na kitengo kinachosimamia mahusiano ya kimataifa katika masuala ya Uchumi na Biashara. Kwa muktadha huo, taasisi hii ni daraja muhimu katika kuunganisha wafanyabiashara wa hapa nchini Urusi na Tanzania.
Lengo hasa la Taasisi ya Business Russia lilikuwa ni kuja kujitambulisha kwa Mhe. Balozi Fredrick I. Kibuta na kueleza utayari wao wa kushirikiana na Ubalozi wa Tanzania katika kukuza uwekezaji na urari wa biashara kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Shirikisho la Urusi hivyo walimkaribisha Mhe. Balozi kushiriki katika jukwaa la biashara litakalofanyika mwezi Aprili 2022.
Mbali na mwaliko huo, wawakilishi wa Business Russia walimuomba Mhe. Balozi kuwapa taarifa za fursa za uwekezaji zilizopo nchini Tanzania ili wazitangaze kwa wawekezaji wa hapa Urusi. Vilevile walieleza kuwa wapo tayari kushirikiana na Ubalozi katika kuratibu majukwaa ya kibiasahara na pia kuratibu ziara za Mhe. Balozi katika majimbo mbalimbali hapa nchini Urusi.
Halikadhalika, wajumbe wao walieleza maeneo muhimu ambayo wanaona kuna fursa kwa ajili ya wawekezaji kutoka nchini Urusi. Fursa za uwekezaji zilizoainishwa ni pamoja na: Uwekezaji wa Miundombinu ya Utalii, Viwanda vya kuunganisha vifaa vya kusafisha maji, Vituo vya ukusanyaji wa bidhaa za kilimo na miundombinu ya kuhifadhi bidhaa hizo kabla ya kusafirishwa. Aidha, walisema kwa sasa wapo kwenye mchakato wa kufungua ofisi ndogo ya kuuza magari aina ya KAMAZ na wanategemea kuja kufanya wasilisho hilo mwezi Julai 2022 wakati wa Maonesho ya Saba saba.
Sambamba na hayo kiongozi wa ujumbe huo alieleza kwamba kwa sasa wapo kwenye hatua ya mazungumzo na Chuo Kikuu cha Dodoma ili kuanzisha idara ya mafunzo ya Lugha ya Kirusi katika chuo hicho. Kiongozi huyo alimkabidhi baadhi ya nakala za kamusi ya “Kiswahili-Kirusi” Mhe. Balozi Fredrick I. Kibuta ili asaidie kuwasilisha kwa uongozi wa Chuo Kikuu cha Dodoma.