Mnamo tarehe 24 Juni 2022 Mhe. Balozi Fredrick I. Kibuta alikutana na uongozi wa juu wa Baraza la Biashara na Viwanda la Jimbo la Kursk (Kursk Chamber of Commerce and Industry) akiwa katika ziara ya kikazi ya siku tatu katika jimbo la Kursk kwa mwaliko wa Gavana wa Jimbo hilo. Miongoni mwa viongozi wa Baraza la Biashara waliohudhuria ni pamoja na Rais wa Baraza la Biashara na Viwanda Kursk, Sergey Nicholaevich, Makamu wa Rais wa Baraza la Biashara na Viwanda Kursk Anna Kostantinovna na Meneja wa Mahusiano ya kikanda na kimataifa wa Baraza hilo Elena Yuryevna.
Mhe. Balozi alielezea kuhusu fursa za uwekezaji zilizopo nchini Tanzania. Maeneo ya uwekezaji yaliyowasilishwa kwao ni ya kilimo, hasa kilimo cha alizeti na uzalishaji wa mafuta ya alizeti. Eneo lingine ni la uzalishaji wa madawa kwa ajili ya matumizi ya binadamu. Aidha, Uongozi wa Baraza hilo umeonekana kuitikia kwa haraka kilimo cha alizeti na uzalishaji wa mafuta ya alizeti. Hivyo, kwa pamoja walikubaliana na kumweleza Mhe. Balozi kuwa Baraza hilo litaandaa ujumbe wa wazalishaji wa mafuta yatokanayo na mimea ambao wapo tayari kuja kukutana na taasisi za kisekta za Tanzania kwa lengo la kupata taarifa zaidi kuhusu miradi iliyopo, taratibu za uwekezaji, ukubwa wa soko (ndani na nje) na maeneo ya uwekezaji katika kilimo cha alizeti. Ujumbe huo unatarajia kuja Tanzania kati ya mwezi Oktoba na Novemba 2022.
Sambamba na hilo uongozi wa baraza la biashara la Kursk ulisema kwamba mpaka sasa Tanzania na jimbo la Kursk hawana mahusiano ya kibiashara. Hivyo, ujio wa Mhe. Balozi umefungua ukurasa mpya na utasaidia kuanzisha mahusiano ya kibiashara kati ya Tanzania na jimbo la Kursk.