Tanzania inatarajiwa kupokea watalii wengi zaidi siku za hivi karibuni kutoka nchini Russia. Tathmini hii imetokana  na mazungumzo yaliyofanyika mnamo tarehe 31 Machi 2022 kati ya Mhe. Balozi Fredrick I. Kibuta na ugeni kutoka Bunge la Shirikisho la Urusi. Ujumbe huo ulikuwa na watu wawili ukiongozwa na Bw. Ammosov Petr Revaldovich ambaye ni mwakilishi wa Jimbo la Skha-Yakutia lililopo Kaskazini mwa Urusi. Bw. Ammosov aliambatana na Bw. Konstantin Nikolaevich ambaye ni msaidizi wake.

 

Lengo la ujio wao pamoja na mambo mengine ilikuwa ni kufahamiana na Mhe.  Balozi mpya wa Tanzania Urusi,ikiwa ni, pamoja na kujadili njia ya kukuza mahusiano ya Kiuchumi na Biashara kati ya nchi za Tanzania na Shirikisho la Urusi hususan  katika Sekta ya Utalii. 

 

Bw. Ammosov alieleza zaidi kuwa kutokana na vikwazo vilivyowekwa na Umoja wa Ulaya na Marekani dhidi ya Urusi, Watalii wengi raia wa Urusi wanatarajiwa kuja Afrika, kwa hiyo Tanzania ijiandae. Vilevile alisema kwamba mambo muhimu ya kuzingatia ni ukweli kwamba, warusi wengi wanapenda kupumzika katika fukwe (beach and resorts), hivyo ni vyema Serikali ya Tanzania ikaandaa mazingira wezeshi kwa ajili ya watalii raia wa Urusi. Hata hivyo alitilia mkazo suala la ulinzi na usalama wa Watalii raia wa Urusi kwamba ni jambo la muhimu.  

Pamoja na mambo mengine, Bw. Ammosov alisema kwamba, ili kuendeleza mahusiano katika ngazi ya jimbo/au mkoa ni vyema serikali ya Tanzania ikaangalia uwezekanao wa kuanzisha mahusiano ya kimiji (Sister City). Kwa mfano, Jimbo la Skha-Yakutia linaweza kuanzisha mahusiano na mkoa wa Arusha au mkoa wa Kilimanjaro ambayo ni mikoa ya Utalii. Vilevile aliwakaribisha watalii raia wa Tanzania kuja kutembelea jimbo lake la Sakha-Yakutia ambalo kwa miaka minne iliyopita imekuwa ikipokea watalii wengi kutoka barani Afrika na nchi zingine duniani. Kivutio kikuu cha Utalii ni kwamba watalii wengi huja kuongelea kwenye maji yenye nyuzi joto hasi sitini na moja (-61 nyuzi joto) kwani jimbo hilo lipo Kaskazini mwa Urusi ambapo kuna Baridi sana. 

Aidha, Mhe. Balozi Fredrick I. Kibuta, kwa upande wake, aliwashukuru wajumbe hao kwa kuitambua Tanzania kama sehemu sahihi na mahali salama kwa ajili ya Watalii raia wa Urusi. Aidha, aliwaeleza kuwa Tanzania ipo tayari kupokea watalii wengi zaidi kwani hali ya hewa ni nzuri na usalama kwa watalii upo. Aidha, aliongeza kuwa Serikali inaendelea kuwekeza kwenye miundombinu wezeshi ya Utalii. Halikadhalika aliwaaihidi kuwapa taarifa mbalimbali kuhusu vivutio vya Utalii vilivyopo nchini Tanzania 

#kaziiendelee 

 

Moscow 

31 Machi 2022