Ubalozi wa Tanzania Moscow waadhimisha Miaka 61 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar katika Ukumbi wa GLAV UPDK CULTURE CENTER, Moscow Urusi ambayo yalienda sambamba na kuienzi lugha ya Kiswahili. Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo alikuwa ni Mhe. Fredrick Ibrahimu Kibuta, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Urusi. Wadau walioshiriki maadhimisho hayo ni Pamoja na Mabalozi wa nchi zinazounda Jumuiya ya Afrika Mashariki na SADC; Wizara ya Mambo ya Nje ya Urusi, Wizara ya Maendeleo ya Biashara na Uchumi ya Urusi; walimu wanaofundisha Kiswahili nchini Urusi ambao pia ni wanachama wa CHAKIMO; Viongozi wa Jumuiya ya Diaspora wa bara la Afrika; Viongozi wa Jumuiya ya Diaspora wa Tanzania wakiwemo wanafunzi; wanafunzi wanaosoma Kiswahili katika vyuo mbalimbali nchini Urusi Pamoja na marafiki wa Tanzania. Katika hatuba yake Mhe. Balozi alizungumzia masuala mbalimbali yakiwemo sababu zilizopelekea Tanganyika na Zanzibar kuungana, Busara za Mheshimiwa Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Aman Abeid Karume katika kufanikisha muungano wetu, namna viongozi wengine wakitaifa wanavyoendelea kuitunza TUNU ya Muungano; nafasi ya lugha ya Kiswahili katika kufanikisha na kudumuisha Muungano Pamoja na mafanikio mengi yaliyopatikana na yanayoendelea kupatikana kupitia Muungano huo.
Sambamba na hilo, Profesa S. Ayvazyan (Mbunge), ambaye aliwahi kuwa Afisa Ubalozi wa Urusi nchini Tanzania katika Miaka ya 1968 hadi 1972, aliwasilisha mada kuhusu Wasilisho kuhusu Mwl. Julius Kambarage Nyerere ambapo aliongelea masuala mengi yakiwemo utendaji kazi wa Mwalimu Nyerere na jitihada zake katika kuikomboa Tanzania na Afrika kwa ujumla. Aidha, Mhe. Dkt. Peter Mathuki, Balozi wa Jamhuri ya Kenya na mwenyekiti wa vikao vya Mabalozi nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika mashariki, alizungumzia kuhusu kukua kwa lugha za Kiswahili katika maeneo mbalimbali ya Afrika. Aidha Mhe. Dkt. Mathuki alipongeza Serikali ya Tanzania kupitia Ubalozi wa Tanzania nchini Urusi kwa namna Ubalozi unavyoshirikiana na CHAKIMO katika kukuza na kueneza Lugha ya Kiswahili.
Vilevile, Warusi wanaozungumza vizuri lugha ya Kiswahili walipata nafasi ya kuonesha matukio mbalimbali ikiwemo kuimba mashairi kwa Kiswahili, kutafsiri hadithi zilizoandikwa kwa Kirusi katika lugha ya Kiswahili; kuimba nyimbo mbalimbali pamoja na mashairi.
Mwisho, mwakilishi wa wanafunzi kutoka Taasisi ya nchi za Asia na Afrika aliwasilisha mada kuhusu ushirikiano na mahusiano mzuri yaliyopo kati ya Tanzania na Urusi ambapo aliainisha masuala mbalimbali ya ushirikiano; Aina ya biashara zinazofanyika kati ya Urusi na Tanzania; kukua kwa biashara; Ongezekano la wanafunzi wanaosoma kwa ufadhili wa Serikali ya Urusi Pamoja na kupanuka kwa ushirikiano wa kitaasisi kati ya Tanzania na Urusi ambao umepelekea ongezeko la utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo nchini Tanzania.
Maadhimisho ya Miaka 61 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar pamoja na kuenzi siku ya Kiswahili Duniani Tarehe 26 Aprili 2025
