Balozi wa Tanzania nchini Russia, Mhe. Fredrick Ibrahim Kibuta amewasilisha Hati za Utambulisho kwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Shirikisho la Urusi anayeshughulikia masuala ya Bara la Afrika, Mhe. Bogdanov Mikhail Leonidovich, katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Shirikisho la Urusi jijini Moscow leo tarehe 10 Machi 2022. Baada ya kuwasilisha Hati hizo, Balozi Kibuta alifanya mazungumzo na Mhe. Naibu Waziri. Loonidovich.

 

Wakati wa Mazungumzo hayo pamoja na mambo mengine, Balozi Kibuta aliishukuru Serikali ya Russia kwa kusaidia kuwanasua wanafunzi 11 waliokuwa wamekwama katika Chuo Kikuu Sumy nchini Ukraine, kufuatia kuibuka kwa mzozo kati ya Shirikisho la Urusi na Jamhuri ya Ukraine. Sambamba na shukrani hizo, Mhe. Balozi Kibuta alimuhakikishia Mhe. Naibu Waziri kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaendelea kushirikiana na Shirikisho la Urusi ili kutekeleza diplomasia ya uchumi kupitia sekta mbalimbali za Ushirikiano. Alimuahidi kuharakisha utiaji saini wa mikataba iliyosalia ili kuwezesha utekelezaji wake kwa manufaa ya pande zote mbili za Ushirikiano. 

Vilevile, Mhe. Balozi Kibuta aliahidi kuwa Tanzania itaendelea kudumisha uhusiano uliopo wa muda mrefu katika nyanja mbalimbali ikiwemo biashara, uwekezaji, utalii , nishati, afya na  elimu pamoja na kufungua milango ya Ushirikiano katika maeneo mengine.

Mhe. Bogdanov alipongeza uhusiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na Shirikisho la Urusi na alisisitiza kuwa Shirikisho la Urusi litaendelea kushirikiana na Tanzania kwenye nyanja mbalimbali. Aidha, alimuhakikishia Mhe. Balozi Kibuta kuwa Serikali ya Russia ipo tayari kutoa Ushirikiano ili aweze kutekeleza majukumu yake kwa wepesi kwa maslahi mapana ya pande zote.